Wednesday, 24 February 2016

VPL AZAM KAZINI LEO DHIDI YA TZ PRISON

MLINZI wa kati, Nurdin Chona atarejea katika kikosi cha Tanzania Prisons baada ya kukosekana katika mchezo uliopita dhidi JKT Mgambo. Chona alikosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano. Prisons itawakabili Azam FC katika mchezo wa ligi kuu Bara.
Mchezo huo wa kiporo utapigwa katika uwanja wa Sokoine, Mbeya leo jioni. Ushindi utawapeleka kikosi cha kocha Salum Mayanga hadi katika nafasi ya nne ya msimamo na itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo ya Mbeya kufika ‘TOP 4’ tangu msimu wa 2007/08 ambao walimaliza katika nafasi ya pili.
Azam inaweza kurudi kileleni kama itapata ushindi katika mchezo huo lakini wanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kupata ushindi wowote dhidi ya Prisons katika uwanja wa Sokoine tangu walipopanda ligi kuu msimu wa 2008/09.
Katika michezo sita iliyopita ya ligi kuu iliyozikutanisha timu hizo mbili, Azam FC imeshinda mara mbili ( 3-0 mwaka 2013, 2-1 mwaka 2015-mechi zote zilichezwa Chamanzi Complex) na mechi nyingine 4 (sare tatu katika uwanja wa Sokoine, sare moja Chamanzi).
Prisons haijapata ushindi wowote katika michezo minne iliyopita, wakati Azam wamepoteza mara mbili katika mechi tano zilizopita.
Jeremiah Juma ndiye mfungaji namba moja wa Tanzania Prisons. Mchezaji huyo tayari amefunga magoli 11 hadi sasa katika ligi kuu amekuwa ‘mwiba mkali’ kwa timu pinzani. Atakutana na walinzi David Mwantika na Mu-ivory Coast, Paschal Wawa lakini bado anaweza kufunga kutokana na usaidizi mzuri ambao amekuwa akiupata kutoka kwa Mohamed Mkopi ambaye tayari amekwishafunga magoli saba hadi sasa.
Mu-ivory Coast, Kipre Tchetche yeye pia ndiye kinara wa Azam katika ufungaji. Amefunga magoli tisa, wakati patna wake na nahodha wa timu, John Bocco yeye amekwishafunga magoli saba. Chona na patna wake James Mwasote watakuwa na mtihani wa kuzuia washambuliaji hao wenye uchu ambao wataongezewa nguvu na kijana Farid Musa.
Juma Seif ‘Kijiko’  Lambert Sibian wataongoza safu ya kiungo ya TP dhidi ya wale wa Azam FC ambao bila shaka wanaweza kuwa Frank Domayo, Salum Abubakary na Himid Mao. Nahodha, Laurian Mpalile na Salum Kimenya watapangwa kama walinzi wa pembeni upande wa Prisons.
Walinzi hao wanapaswa kuwa makini na mchezo wao wa kupanda sana mbele kusaidia mashambulizi kwani Shomari Kapombe na Erasto Nyoni pia wamekuwa sababu ya matokeo mazuri ya kikosi cha Muingereza, Stewart Hall.
Walinzi hao wa pembeni pia wamekuwa na kawaida ya kupanda mbele kusaidia mashambulizi huku Kapombe akiwa hatari katika ufungaji na utoaji wa pasi za mwisho. Mlinzi huyo wa kulia wa Azam tayari amefunga magoli saba katika VPL msimu huu.

No comments:

Post a Comment